Mwanzo » » MAITI YAFUKULIWA NA KUKATWA KICHWA

MAITI YAFUKULIWA NA KUKATWA KICHWA

Imewekwa ma Unknown siku Wednesday, 16 October 2013 | 11:56



HOFU imezidi kutanda miongoni mwa wakazi wa mji wa Geita, baada ya watu wasiojulikana kufukua kaburi, kisha kukata kichwa cha maiti iliyokuwemo na kuondoka nacho. Tukio hilo la kusikitisha na ambalo halipaswi kufumbiwa macho, lilitokea jana katika makaburi yaliyopo Mtaa wa Elimu Nyantorotoro, mkoani hapa.

Tukio hilo ambalo limeshuhudiwa na umati mkubwa, limekuja siku chache wakati wakazi wa mji huo wakiwa na hofu, baada ya kutokea tukio la mtoto Shaabani Maulidi (16), aliyefariki miaka zaidi ya miwili iliyopita na kuonekana akiwa hai jirani na mtaa huo.

Watu hao, ambao walipasua sanduku la maiti na baadaye kutoa kichwa cha maiti hiyo ya mwanamume ambayo jina lake halikufahamika, waliacha kaburi wazi bila kulifukia.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu Nyankumbu, Hassan Malima, tukio hilo liligunduliwa saa tatu asubuhi na watu waliokwenda eneo hilo kuchimba kaburi, baada ya kutokea msiba kwa Mchungaji Mtafuten Mihana wa Kanisa la PEFA, aliyefiwa na mtoto wake, Rebeka (28).

"Tulipofika katika eneo hilo tukiangalia sehemu ya kuchimba kaburi kwa ajili ya huyo marehemu mtoto wa mchungaji, ndipo tukaona hilo kaburi likiwa limefukuliwa, tuliposogea tukashuhudia maiti ikiwa imekatwa kichwa," alisema mwenyekiti huyo.

Inasemekana kaburi hilo limefukuliwa majira ya usiku wa kuamkia jana na kwamba maiti iliyokuwemo inadaiwa kuwa imezikwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita, ingawa ndugu hawakujulikana kutambua hali hiyo.

Uongozi wa mtaa huo baada ya kupata taarifa za tukio hilo, linalohusishwa na imani za kishirikina, walitoa taarifa polisi, ambao walifika eneo la tukio, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Geita (OCD), Bwire.

Polisi kwa kushirikiana na wananchi, walifukua kaburi hilo ili kutambua jinsia ya maiti hiyo, ambayo ilijulikana kuwa ni ya kiume.

Mchungaji wa Kanisa la PEFA katika mtaa huo, Mtafuten, alisema tukio hilo ni la imani za kishirikiana, kutokana na wananchi kukosa imani na kuamini kutumia njia hiyo wanaweza kufanikiwa katika maisha yao.

Alisema watu wamekosa imani ya Mungu na kwamba wanadiriki kuchukua viungo vya watu waliokufa na kuzikwa, hivyo amewataka watu kuachana na imani za kishirikina na badala yake wamtegemee Mwenyezi Mungu pekee watafanikiwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita (RPC), Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba uchunguzi bado unaendelea.
Share habari hii :

Post a Comment

WADHAMINI WA BLOG YETU

SIKILIZA CLOUDS FM ONLINE HAPA

TUFUATE HAPA

WASOMAJI WETU

FACEBOOK

DONDOO ZA MWEZI

TWITTER

BLOG ZA WADAU

 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
HAKIMILIKI © 2013. CLICK BONGO TZ - Haki zote zimehifadhiwa